Jun 27, 2014

‘TRA Bara wanasababisha mgogoro’

SALEEEL
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Omar Yussuf Mzee, amesema watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) upande wa Tanzania Bara,wanasababisha mgogoro wa makusudi kwa wafanyabiashara wa Zanzibar.

Akitoa ufafanuzi kuhusu hoja ya Mwakilishi wa Kikwajuni, Mhe. Mahmoud Mohammed Mussa, kuhusu makontena ya Zanzibar yaliyozuiliwa bandarini Dar es Salaam na kitendo cha kuletwa wafanyakazi saba wa TRA kufuatilia makontena hayo wakati akichangia bajeti ya wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Waziri huyo alisema TRA Tanzania Bara wana tatizo lakini hawalisemi, hali inayosababisha mgogoro mkubwa.

Hata hivyo, alisema wataendelea kutafuta kiini cha tatizo hilo kwa mazungumzo na ikishindikana watatumia Kamati ya kero za Muungano.

Aidha alisema wizara inasubiri majibu kutoka TRA Zanzibar kuhusu wafanyakazi wa TRA Tanzania Bara kutumwa kuchunguza makontena hayo, baada ya kupokea malalamiko kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenyeviwanda na Wakulima (ZNCCIA) kuhusu kitendo hicho cha TRA.

Mapema Mbunge huyo wa Kikwajuni, alisema wafanyakazi hao wa TRA walitumwa kufuatilia makontena hayo na kuyapekuwa kujua kilichomo ndani na kuripoti makao makuu na kuhoji utaratibu huo utaendelea hadi lini.

Alisema makontena hayo yalifika bandarini Dar es Salaam tokea Juni 5, lakini yalikuwa yakizuiliwa na TRA kwa utashi wao tu na kwa lengo la kudhoofisha biashara ya Zanzibar.

Wakichagia bajeti hiyo,Wawakilishi walieleza kusikitishwa kwao kufa kwa viwanda vya ndani, hali iliyosababisha ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana.

Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Mhe. Saleh Nassor Juma, alisema Zanzibar ilikuwa na viwanda vingi muda mfupi baada ya mapinduzi, lakini vyote vimekufa na kudhoofisha mfumo wa ajira kwa vijana.

Aidha aliitaka wizara hiyo kutafuta ufumbuzi wa moshi nzito unaotoka katika kiwanda cha makonyo Wawi, ambao unasababisha athari za kiafya kwa wananchi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo Tumbe, Mhe.Rufai Said Rufai, aliitaka serikali kuimarisha viwanda ili kukuza uchumi.

Akitoa majumuisho, Naibu Waziri wa Viwanda, Mhe. Thuwaiba Kisasi, aliwataka wafanyabiashara kuwa na moyo wa huruma kwa wananchi katika kipindi hichi wakijiandaa na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Alisema serikali ilitoa msamaha wa kodi kwa wafanyabiashara wa chakula, kwa lengo la kuuza bidhaa zao kwa wananchi kwa bei nafuu, lakini misamaha hiyo hawaisaidii walaji na kuendelea kununua bidhaa kwa bei ya juu.

Kuhusu kodi mara mbili, Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, alisema bado tatizo hilo linaendelea kwa wafanyabiashara wa Zanzibar.

Alisema wapo baadhi ya wafanyakazi wa TRA ambao kwa makusudi wanataka kudhoofisha Muungano na kufanya ubaguzi baina ya wafanyabiashara wa Zanzibar na Tanzania Bara jambo ambalo halifai kwani linaweza kuleta athari kubwa siku za baadae.

Kuhusu kufungwa kiwanda cha kuzalisha vinywaji baridi cha Coca Cola Zanzibar, alisema kiwanda hicho kimesitisha uzalishaji kutokana na mitambo yake kuchakaa na hofu waliyonayo wamiliki wa kampuni hiyo kwamba kikiachiwa kuendelea kuzalisha kinaweza kuzalisha bidhaa zisizo na ubora.

Hata hivyo, aliwatoa hofu Wawakilishi kwamba serikali inaendelea kuzungumza na uongozi wa kiwanda hicho na kwamba mitambo iliyopo ndani ya kiwanda hicho ni mali ya kampuni lakini majengo ni ya serikali.

Hivyo, kama kampuni hiyo itashindwa kufanya uzalishaji, serikali itatafuta mwekezaji mwengine.
Wajumbe wa baraza hilo walichangia bajeti ya wizara hiyo baadae wakaipitisha.

0 comments:

Post a Comment